Kinyozi anapokosea kukunyoa bila kujali amekosea kiasi gani siku zote baada ya muda Fulani nywele huota tena na utaweza kunyoa vile unavyotaka. Unapopoteza fedha haijalishi ni nyingi kiasi gani kama ni wewe mwenyewe ulizitafuta basi utaweza kuzipata tena.

Unapoachwa na mpenzi ambaye ulimpenda sana bila kujali alikuwa mzuri kiasi gani, bado ipo siku utakuja kukutana na mtu mwingine mzuri kuliko yeye na utampenda kuliko yeye. Ni wewe tu kuamua kwamba yaliyopita yapite uendelee na safari.

Kipo kitu kimoja kikitokea kwenye Maisha yako huwezi kubadilisha tena, kitu hicho ni KIFO. Unapokufa inakuwa ndio mwisho wako wa kufanya vitu hapa duniani. Huwezi tena kurudi kuja kubadilisha chochote. Na bahati mbaya sana baada ya kufa hakuna ajuae kinachoendelea au mtu anakuwa wapi.

Sasa nikuombe wewe ambaye upo hai usikubali jambo lolote ambalo linaweza kubadilishwa likuumize kichwa au likufanye ukate tamaa. Nataka ukumbuke kwamba ipo siku utakufa na hutopata tena hiyo nafasi ya kuanza upya uliyonayo sasa.

Dunia haina shida wala haijutii wewe ukifariki, kila siku wanazaliwa watu wapya ambao watakuja kufanya kile ambacho wewe ulishindwa kufanya. Sasa usikubali kuondoka hivi hivi, usikubali alama uliyotakiwa kuiacha ije iachwe na mtu mwingine.

Ndugu yangu kinyozi akikosea kukunyoa kumbuka kwamba nywele zitaota ten ana utakuja kurekebisha vile unavyotaka. Lakini siku ukiondoka ndio inakuwa imekwisha hakuna kingine utakachoweza kufanya. Hivyo basi nikukumbushe tena usikubali kuacha kutumia nafasi yoyote inayokuja mbele yako ambayo inakuwezesha wewe kufika kule unakotaka. Usikubali kukata tamaa na kusema haiwezekani na wakati bado upo hai.

Nakutakia Kila La Kheri.

Kupata huduma na Bidhaa mbalimbali kwenye mtandao huu bonyeza linki hii www.jacobmushi.com/kocha

Makala hii imeandikwa na Kocha Jacob Mushi. Mwandishi wa Vitabu na Makala, Kocha wa Maisha, na Mjasiriamali.

Andika Maoni Yako Hapa

Discover more from Jacob Mushi

Subscribe now to keep reading and get access to the full archive.

Continue reading