Habari za leo Rafiki yangu. Natumaini unaendelea vyema katika kupambana na maisha. Leo ninataka ufahamu jinsi mimi nilivyoanza safari hii ninayoendelea nayo. Safari ya kufundisha na kuhamasisha wengine wafikie mafanikio.
Mwaka 2010 nilikua na marafiki zangu wawili Samweli Lyatuu na Steven Mshiu marafiki hawa tulikua tunasali pamoja na wakati mwingine tunalala pamoja. Mara nyingi ukiwauliza hata sasa watakwambia kwamba nilikua nazungumza sana mambo ya mafanikio wakati nikiwa nao. Pia nilikua nikiwaeleza kwamba hua najiona nikiwa juu sana kwenye mafanikio, najiona kama mtu anaejulikana sana na wengi. Kipindi hicho sikuwahi kutambua nifanye nini ili niweze kuifikia ndoto yangu hiyo. Sikuwahi kupata mtu wa kunishauri ni njia gani niitumie ili kufikia ndoto hiyo. Lakini siku zote nilikua nazungumza na kuwaambia hao marafiki zangu.
 Kipindi hicho pia nilikua napenda sana kufuatilia siasa hivyo nikawa nawaza laba nitakuja kuwa mwanasiasa.  Nikawa najiona nimekua mbunge nazungumza bungeni. Nikawaza pia kuwa raisi wa nchi. Bila kusahau pia nilikua mpiga kinanda kanisani kwetu hivyo pia nikawa najiona kama mpiga kinanda maarufu sana hapa Tanzania. Nikajikuta napenda kufanya vitu vingi lakini sipati furaha ndani ya moyo wangu. Kuna kipindi pia nilijiona nimekua muigizaji nikaanza kumfuatilia Kanumba na kuwaza siku moja nitakutana nae. Sikuwahi kuwaza kua na pesa nyingi Zaidi niliwaza kujulikana na watu wengi duniani. Kipindi hicho habari za freemason ndio zilikua zinapamba moto hivyo zikaanza kututia hofu na nikafikiri labda wataanza kunifuatilia na mimi.
Lakini nilikuja kugundua kitu siku moja kwamba mara nyingi kila kitu kipya ninachokijua hua nawaelezea wenzangu. Nikipata wazo jipya ninawaelezea. Siku moja tukaungana pamoja tukaanzisha kikundi kinaitwa Rise & Shine kikundi hiki tulikusudia kukitumia ili kila mmoja aweze kufanya kile anachokipenda. Wakati huo rafiki yangu Samwel alikua na huduma ya uimbaji kanisani. Hivyo yeye tayari alishajua kwanini yupo duniani. Rafiki yangu Steven yeye alikua anapenda kufundisha kanisani. Mimi nilikua napenda kuzungumzia Zaidi juu ya kufanikiwa na kufikia ulimwengu Zaidi. Sikuwahi kufahamu juu ya Wahamasishaji wala majukwaa mengine ambayo mtu anaweza kusimama na kufundisha. Nilikua nafahamu tu juu ya Wahubiri makanisani, Waalimu, Wachungaji, Wainjilisti na Maaskofu. Nikiwaza nafasi hizi nikajiona hazinitoshi kabisa kufikia ile ndoto ninayoiona.
Hali ya kugundua ni kitu gani hasa natakiwa nifanye ili nitimize ndoto yangu ilinitesa sana kwasababu kila ninachokutana nacho najiona nipo juu na nimefikia mafanikio. Nakumbuka kuna siku mtu mmoja alinishauri nikasomee uaskari baada ya matokeo yangu ya kidato cha nne kutokuruhusu kwenda Advance. Hapo nikaanza kujiona nikiwa IGP nikaanza kujiona mtu mkuu kwenye nchi hii na watu wananisikiliza lakini moyo wangu haukubali kwasababu nilikua nawahurumia watu. Nikaona nafasi hiyo itanifanya niwe nawaumiza wengine. Hapa utakuja kugundua kwamba mtu yuko vile alivyo kutokana na vile vitu alivyokua anavifuatilia mara kwa mara.
Mwaka 2012 nikaenda kujifunza kozi ya IT (Information Technology) nikaanza kuwaza kuwa hacker bora Zaidi hapa Tanzania lakini sikuweza kuifanya vizuri. Sababu kubwa ni kwamba nilikua sifurahii vyote hivyo katika moyo wangu. Kuna vitu unaweza kuvifanya ukatimiza ndoto yako lakini moyoni mwako unaumia. Inawezekana umewaumiza wengine wengi ili ndoto yako itimie hovyo huwezi kupata furaha kabisa.
Mwaka 2014 nilianza kusoma vitabu ndipo nikakutana na watu wanaowafundisha wengine juu ya mafanikio. Hapo ndipo nilipogundua kitu kilichokuwa ndani yangu. Nikajikuta natamani sana kuona watu wengi wakifanikiwa kwa kuyatendea kazi yale ninayoyasema na kuyaandika. Nikaanza kutamani na mimi siku moja niwe Mwandishi wa vitabu vingi kama wengine. Ninaweza kukwambia kwamba hapo ndipo nilipoanza kuona njia ya kuelekea kule ninapokua napatamani kufika yaani kwenye ndoto zangu.
Hata wewe Unaweza Kuanza Sasa.
Embu jiulize leo ni kitu gani siku ukiondoka duniani utajuta sana kwa kutokukikamilisha?
Ni kitu gani Hasa unafikiri ukikifanya moyo wako ndio unapata furaha kutoka ndani?
Jaribu kuiona dunia ukiwa haupo duniani, angalia ni kitu gani kinakosekana hapa duniani wewe usipokuwepo kisha urudi katika hali yako ya kawaida uanze kukifanya hicho kitu. Ili kugundua kusudi lako kunahitaji utulivu, muda, nafasi na kujifunza pia. Hii ni kwasababu tulizaliwa bila kujua chochote lakini tunaendelea kugundua vitu vingi ndani yetu kila siku.
Haijalishi hadi sasa una miaka mingapi inawezekana leo ukagundua kusudi lako na ukaliishi. Ndio maana nimeandika kitabu kinaitwa Siri 7 za Kuwa Hai Leo kwa maana kwamba haijalishi una umri gani hata kama ni mzee kabisa kuwepo kwako hai leo kuna jambo unatakiwa ulikamilishe.
Nafurahi sasa kuona na wewe rafiki yangu umeamua kuniunga mkono kwa kujiunga na Blog hii ili ujifunze na upate mafanikio. Mafanikio yangu mimi ni pale ninaposikia kuna mtu/watu wameweza kupiga hatua Fulani kwenye maisha yao kupitia Makala, na vitabu ninavyoviandika. Nashukuru sana pia kwa kuweza kuniamini na kuweka email yako kwenye mtandao huu ili upokee mafunzo haya kwa njia ya email. Karibu sana Tufanye kazi pamoja ili tufikie mafanikio makubwa.
 

Andika Maoni Yako Hapa

Discover more from Jacob Mushi

Subscribe now to keep reading and get access to the full archive.

Continue reading